Tuesday, August 27, 2013

WAKAZI WA MIVINJENI WASHINIKIZA MALIPO YAO

 WAKAZI wa Mivinjeni Kurasini wanaotakiwa kuhama kupisha mradi wa  uwekezaji wa EPZ wamefunga barabara kuishinikiza Serikali kuwalipa hundi zao na si viwanja. Hali hiyo ilijitokeza leo jijini  Dar es Salaam Majira ya Saa tano asubuhi ambapo wananchi walijipanga barabarani na kuzuia magari kupita kuishinikiza serikali kuwalipa fidia ili waweze kuondoka katika eneo hilo.

Akizungumza katika eneo hilo  Katibu anayefutilia malipo ya wakazi hao Judith George alisema kuwa  wakazi hao wamelala  barabarani kutokana na serikali kuwapiga dana dana kulipwa hundi za nyumba zao ili waweze kuhama.

Alisema kuwa Viongozi wa Serikali pamoja na Mwekezaji  (EPZ) walifika katika eneo hilo March 13 mwaka huu na kufanya mkutano na wananchi kuhusu  uwekezaji katika eneo hilo.

WANAFUNZI WOTE WAMEFELI LINERIA


Kwa mara ya kwanza katika historia ya Liberia, wanafunzi wote wamefeli mtihani wao wa mwisho wa sekondari na hivyo kumaanisha kuwa hakuna hata mmoja ambaye atafuzu kuingia chuo kikuu. Waziri wa elimu wa Liberia amesema ameshinda kufahamu ni kwa nini hakuna wanafunzi hao wamefeli kiasi hicho.

Zaidi ya wanafunzi elfu ishirini na watano walianguka mtihani huo ambao ungewapa fursa ya kujiunga na chuo kikuu cha Liberia ambacho ni moja ya vyuo vikuu vinavyoendesha na serikali.

Lakini wasimamizi wa chuo hicho wameiambia BBC kuwa wanafunzi hao hawakuwa makini na ufahamu mzuri wa lugha ya Kiingereza ambayo ilitumiwa kuwatahini. Taifa la Liberia linaendelea kujinasua kutokana na athari za mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyomalizika zaidi ya miaka kumi iliyopita.

MWEKEZAJI AHADI USALAMA UWANJA WA NDEGE




Dar es Salaam. Mwekezaji Sheikh Salim Abdullah ametangaza kuwekeza kwenye Uwanja Wa Ndege wa Kimataifa wa JK Nyerere Dar es Salaam (JNIA) kwa kufunga mashine za kisasa, ili kuimarisha usalama katika eneo hilo. 

Sheikh Abdullah ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Maendeleo na Uwekezaji ya Al-Harathy ya Oman, alitangaza hatua yake hiyo jana, baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya uwanja huo, ambapo alisisitiza mashine zilizopo uwanjani hapo kwa sasa uwezo wake kiutendaji na kiusalama ni mdogo. “ Mashine hizi uwezo wake ni mdogo, dunia tunayoishi sasa imetawaliwa na magaidi uwanja wa ndege ni eneo muhimu ambalo linapaswa kulindwa kwa uhakika, mizigo inabidi kukaguliwa kwa umakini zaidi kwani wanaweza kuweka mabomu au vitu vingine vya hatari wakasababisha madhara makubwa alisema na kuongeza:

“Nimekuja kuwekeza hapa kwa kuitikia mwito wa Rais Jakaya Kikwete, amechoka sana inabidi sisi tumsaidie, ana nia nzuri ya kuhakikisha nchi hii inakuwa kiuchumi inabidi tumsaidie kuwekeza katika maeneo kama haya” alisema. Katika hatua nyingine mwekezaji huyo ametangaza kuwekeza ndege nane kwenye Shirika la Ndege la Tanzania(ATCL), mradi ambao unatarajiwa kugharimu dola za Marekani 100 milioni.

“ Tunanunua ndege nane ambapo nne ni aina ya Embraer ERJ-175 za Brazil na nyingine nne aina ya Mbombardier,kwa kuanzia tunapeleka vijana 10 wa kitanzania kwenda kusomea jinsi ya kuongoza ndege hizo” alisema. Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Kapteni Milton Lazaro, alieleza kuwa hatua hiyo ni faraja kubwa kwao na wana tumaini itatumiwa vyema kwa manufaa ya kukuza uchumi .

Kwa upande wake,, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alisema Serikali imefanya kazi kubwa kuvutia wawekezaji hao, ikiwa ni pamoja na kusafisha madeni yaliyokuwepo awali

WANAJESHI WA UN WASOMBWA NA MAJI DARFUR


Wanajeshi wanne wa kutunza amani wa Umoja katika eneo la Darfur nchini Sudan hawajulikani waliko baada ya kusombwa na mafuriko. Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa, Rania AbdulRahman, amesema kuwa wanajshi hao walikuwa wakisindikiza msafara wa magari ya kutoa misaada, wakati waliposombwa na maji.

Afisa huyo amesema kuwa wanajeshi wengine wawili walipatikana wakiwa hai na kundi la uokoaji Shirika la Umoja wa Mataifa wa Afya Duniani WHO, limesema kuwa zaidi ya watu laki tatu nchini Sudan, wameathiriwa na mafuriko na zaidi ya watu hamsini wamefariki mwezi huu.

Shirika hilo limesema kuwa eneo linalokaribia mji mkuu wa Khartoum ndilo limeathirika zaidi na mafuriko hayo ambayo ndiyo mabaya zaidi kuwahi kukumba eneo hilo kwa zaidi ya miaka ishirini na mitano iliyopita.
Wanajeshi wakwama kwenye mto

Kikosi cha Umoja wa Mataifa na kile cha Muungano wa Afrika katika eneo hilo la Darfur, UNAMID, ndilo kubwa zaidi duniani na lina zaidi ya wanajeshi elfu ishirini.


Wanajeshi hao wa kutunza amani walikuwa wakielekea eneo la Misterei, takriban kilomita hamsini, Kusini Magharibi mwa mji mkuu wa eneo hilo Geneina, na msafara wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, wakati msafara wao uliposomba na mafuriko.

Msemaji wa WFP Amor Almagro amethibitisha kuwa wafanyakazi wa shirika hilo la WFP waliokuwa kwenye msafara huo, watano kati yao raia wa Sudan na wawili wa mataifa ya Kigeni wako salama. Umoja wa Mataifa haujatoa majina au uraia wa wanajeshi hao ambao hawajulikani waliko.

Mwaka uliopita, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, alilieleza baraza la usalama la Umoja huo kuwa wanajeshi watatu kutoka Tanzania walizama majini baada ya gari lao la kijeshi, kukwama katika mto mmoja nchini Sudan.

Katibu huyo mkuu vile vile alilieleza baraza hilo kuwa kikosi chake nchini Sudan kinakabiliwa na upungufu wa vifaa vya kutosha na vya kisasa, hali ambayo inaadhiriwa juhudi zao za kutunza amani katika eneo hilo la Darfur.

Wanajeshi hao wa Umoja wa Mataifa, wako katika eneo hilo la Darfur, kujaribu kumaliza mzozo uliodumu kwa miongo kadhaa kati ya wanajeshi wa serikali na waasi. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu laki tatu wameuawa kwenye mzozo huo wa Darfur.

CCM YAMTIMUA UWAKILISHI MANSOUR


Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (Nec), jana iliridhia kumvua uanachama, Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi, Mansour Yussuf Himid kutokana na kukiuka miiko ya chama hicho. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuwa Mansour ambaye hivi karibuni alikuwa waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), amefukuzwa uanachama kutokana na kukiuka mambo matatu.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kushindwa kutimiza malengo ya CCM na kutekeleza malengo ya uanachama, kushindwa kutekeleza wajibu wa uanachama na kukiuka maadili ya uongozi, kuikana na kuisaliti Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015. Kutokana na uamuzi huo, Nape alisema Mansour hatakuwa na nafasi ya kukata rufani mahali popote kwa kuwa uamuzi uliofikiwa jana ni wa kikao cha juu cha mwisho.

URUSSI YAONYA MASHAMBULIZI


Serikali za Urussi na Uchina, kwa mara nyingine tena zimetoa onyo dhidi ya kutumia nguvu za kijeshi kutatua mzozo wa kisiasa unaokumba taifa la Syria. Onyo hilo limetolewa huku Marekani na washirika wake wakijadili uwezekano wa kuanzisha mashambulio dhidi ya Syria, kujibu shambulio lililotokea wiki iliyopita.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Urussi amesema, jaribio lolote la kutoshirikisha baraza la usalama la Marekani na kubuni kila alichokitaja kama visingizio ambavyo havina msingi, litakuwa na athari kubwa katika mzozo huo.

Wednesday, August 21, 2013

BROTHERHOOD YALAANI KUKAMATWA KWA KIONGOZI WAKE



Vugu vugu la Muslim Brotherhood limelaani kukamatwa kwa kiongozi wake Mkuu Mohammed Badie, kwa tuhuma za kuchochea ghasia na mauaji.Msemaji wa kundi hilo amesema kukamatwa kwa kiongozi huyo ni njama ya kulipiza kisasi mapinduzi ya umma yaliyomuondoa madarakani Rais wa zamani Hosni Mubarak mwaka wa 2011. Badie alikamatwa na maafisa wa polisi kutoka makaazi yake karibu na kitovu cha maandamano ya wafuasi wa Brotherhood Mjini Cairo.

Jeshi la Misri lilivunja kambi hizo wiki jana ambapo kulitokea maafa ya raia wengi. Wakati huo huo Aliyekua Makamu wa Rais Mohamed ElBaradei anakabiliwa na mashtaka ya kusaliti imani ya taifa.

Bw ElBaradei aliondoka nchini Misri baada ya kujiuzulu kufuatia hatua ya jeshi kuvunja kambi za wapinzani na kusababisha maafa ya mamia ya watu.Utawala wa mpito umetangaza hali ya hatari nchini Misri na kumekua na operesheni kali dhidi ya wafuasi wa Rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Morsi.

KENYA YASAINI DOLA BILIONI TANO


Kenya imesaini mkataba na China ambao unatoa dola bilioni tano kuimarisha huduma za Reli,Kawi na Uhifadhi wa Wanyama Pori kwa taifa hilo la Afrika Mashariki.Makubaliano hayo yaliafikiwa katika ziara ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta nchini China.

Hii ndio ziara ya kwanza ya Rais Kenyatta tangu kuchaguliwa hapo mwezi Machi mwaka huu.Serikali ya Kenya imepongeza mkataba huo na kusema utasaidia nchi kukua kiuchumi na kuboresha maisha ya raia wake.Mwenyeji wa Kenyatta, Rais wa ChinaXi Jinping , ameelezea kuridhishwa kwake na juhudi za serikali ya Bw Kenyatta katika kuimarisha taifa la Kenya.

Tuesday, August 20, 2013

MWANAMKE MWENYE NYWELE NDEFU DUNIANI


MWANAMKE anayetambulika kwa jina la Asha Mandela anaongoza kwa kuwa na rasta ndefu zaidi duniani zenye urefu wa futi 55.

Mwanamke huyo ambaye anadaiwa kuonywa na madakati juu ya urefu wa nywele zake unaweza kumsababishia tatizo la kupooza Asha amedai hawezi kuzikata nywele hizo.

Mama huyo aishiye Atlanta mwenye umri wa miaka 47 anayeweka rekodi ya kuwa na rasta ndefu duniani ameweka wazi humchukua siku mbili kuosha pamoja na kuzikausha nywele zake.

Katika moja ya mahojiano aliyowahi kufanya mwanamke huyo ameeleza kuwa nywele zake zimekuwa ni sehemu ya maisha yake na hatoweza kuzikata kwani akifanya hivyo ni sawa na kujiuua.

SERIKALI YATOA TAKWIMU WAFUNGWA DAWA ZA KULEVYA

SERIKALI imetoa takwimu za mahabusi waliohukumiwa kwa kesi ya dawa za kulevya ambapo takwimu hiyo inaonyesha jumla ya watu 10 wamehukumiwa kwa kipindi cha mwaka 2010,2012.

Hayo yamesemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Assah Mwambene leo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara hiyo.

Monday, August 19, 2013

MAAFISA 24 WA POLISI WAUWAWA



Takriban maafisa 24 wa polisi kutoka Misri wameuawa kwenye shambulizi la kuvizia katika eneo la Rasi la Sinai. Duru zinaarifu polisi hao walikuwa kwenye msafara wa mabasi mawili yaliyoshambuliwa na kundi la watu waliokua na silaha karibu na mji wa Rafa mpaka na Ukanda na Gaza.

Polisi watatu walijeruhiwa kwenye shambulio hilo. Katika siku za karibuni jeshi la Misri limeimarisha operesheni dhidi ya wanamgambo eneo la Sinai hususan baada ya mashambulizi kuongezeka tangu kuanguka kwa uliokua utawala wa Hosni Mubarak mwaka 2011.

Wednesday, August 14, 2013

"HATUNA IMANI NA UCHUNGUZI KUHUSU PONDA



Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania umesema hauna imani na tume iliyoundwa na jeshi la polisi nchini humo kwa ajili ya kuchunguza tukio la kupigwa risasi kiongozi wa kidini Sheikh Ponda Issa Ponda. Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Baruan Muhuza Mratibu wa mtandao huo Onesmo Ole Ngurumwa amewaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam leo kuwa jeshi hilo halina haki ya kujiundia tume ikiwa lenyewe ndiyo linatuhumiwa kumpiga risasi sheikh huyo.

Ngurumwa amesema kuwa inasikitisha kuona vyombo vya dola vinaendelea na uvunjaji wa sheria kwa kutumia nguvu inayokiuka haki za msingi za binadamu. Msemaji wa Jeshi la polisi nchini humo Advera Senso ameiambia BBC mjini Dar es Salaam kuwa jeshi lake kwa kushirikiana na jukwaa la haki jinai wameunda kikosi kazi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tukio hilo huku akikana kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi na polisi.

Senso amewalaumu wafuasi wa Sheikh Ponda kwa kuwazuia askari kumkamata Sheikh huyo kwa kuwarushia mawe, hatua iliyosababisha askari hao kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya na hata hivyo wafuasi hao walifanikiwa kumtorosha kiongozi huyo wa kidini. Mapema Jumatatu asubuhi Baraza la waisilamu Tanzania-BAKWATA limeunga mkono kauli ya Jumuiya ya taasisi za kisilamu na kuitaka serikali kuchunguza kwa kina tukio lililosababisha kupigwa risasi kwa Katibu huyo wa Shura ya Maimamu nchini humo.

Kaimu Sheikh Mkuu wa Tanzania Alhad Mussa Salum amezungumza na waandishi wa habari Mjini Dar es Salaam na kusema kuwa japokuwa BAKWATA imekuwa ikipingana na misimamo ya Sheikh Ponda limesema serikali ilikuwa na nafasi ya kumkamata Ponda kwa kufuata mkondo wa sheria. Sheikh Ponda amekuwa katika mivutano ya mara kwa mara na serikali ya Tanzania, anadaiwa kupigwa risasi baada ya kutokea vurugu kwenye mkutano wa mawaidha ya baraza la sikukuu ya Idd el Fitr Jumamosi jioni.

Awali siku ya Jumapili Mwenyekiti wa Shura ya Maimamu Tanzania, Alhajj Mussa Kundecha, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam kuwa endapo serikali haitachukua hatua itakayowaridhisha Waislamu, wataamua kufikiria upya mustakabali wao na serikali ya nchi hiyo.Sheikh Ponda amelazwa katika hospitali ya Taifa, Muhimbili, mjini Dar es Salaam akiuguza jeraha la risasi huku akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu.

Taarifa za jumuiya hiyo ambayo inajulikana zaidi Tanzania kama Shura ya Maimamu zinasema kuwa Sheikh Ponda ambaye polisi wanasema walikuwa wakimtafuta kwa tuhuma za kutoa matamko ya uchochezi, alisafirishwa usiku kutoka mji wa Morogoro hadi Dar es Salaam zaidi ya kilomita 200.Sheikh Ponda kwa sasa anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja alichohukumiwa mapema mwaka huu baada ya kukutwa na makosa kadhaa ikiwemo uchochezi wa kuharibu mali za watu.

DAKTARI AIBA HEROIN TUMBONI MWA MGONJWA


Polisi nchini Urusi wamemzuilia daktari mmoja mpasuaji kwa madai ya kuiba kifuko kilichokuwa na dawa ya kulevya ya Heroin kutoka tumboni mwa mgonjwa. Polisi katika eneo la Siberian walimtaka daktari kumfanyia upasuaji mshukiwa ili waweze kunasa dawa hiyo ambayo mgonjwa alikuwa ameimeza. Hata hivyo polisi waligundua kuwa seheme ya dawa hiyo iliyotolewa tumboni mwa mshukiwa ilikuwa inakosekana

Maafisa wa utawala wanadai kuwa daktari huyo alikuwa mlevi walipomkamata. Huenda akafungwa jela kwa miaka 15 ikiwa atapatikana na hatia ya wizi wa dawa za kulevya.

MUGABE AWAPIGA VIJEMBE WAPINZANI


Rais aliyechaguliwa tena kutawala kwa muhula mwingine nchini Zimbabwe Robert Mugabe, amewaambia wapinzani wake kwenye uchaguzi uliokamilika hivi karubini kuwa ikiwa hawajapendezwa na matokeo ya uchaguzi basi 'wajinyonge'.

Mugabe aliongeza kuwa hawezi kurudi kwenye serikali ya muungano iliyoafikiwa kutokana na vurugu zilizofuata uchaguzi mkuu wa mwaka 2008.Morgan Tsvangirai, anayeongoza chama cha upinzani MDC, alisusia sherehe hizo ambapo Mugabe alitoa hotuba yake ya kwanza tangu kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 31 mwezi Julai.Mugabe aliyatoa matamshi yake makali kwenye sherehe za kuadhimisha siku ya mashuja waliopigania uhuru wa Zimbabwe.

MDC kimewasilisha malalamiko yake mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu hali ambayo imesababisha kucheleweshwa kuapishwa kwa Mugabe. Alishinda uchaguzi huo kwa asilimia sitini ya kuza zote. Hata hivyo majaji wengi wanasemekana kumuunga mkono Mugabe kwa hivyo huenda kesi ya MDC ikatupiliwa mbali.

Chama cha Mugabe Zanu-PF kilishinda wingi wa viti vya bunge kikipata zaidi ya thuluthi mbili ikiwa ni viti 160 ya viti kati ya 210 vya bunge zima.Sherehe za kuadhimisha siku ya mashujaa Zimbabwe, ni sherehe za kujivunia kwa wazimbabwe wakati ambapo nchi hiyo ilijipatia uhuru wake miaka ya sabini.

Hii leo Mugabe ameitoa hotuba yake ya kwanza katika eneo la kumbukumbu la vita hivyo na ambako baadhi ya wapigania uhuru wamezikwa.Hotuba za Mugabe zinasifika zaidi kwa siasa zake kali za kizalendo, na ambazo zaidi hulenga mkoloni wake wa zamani Uingereza na pia anatarajiwa kujipiga kifua kufuatia ushindi wake mkubwa katika uchaguzi mkuu uliopita mwezi jana.

Chama cha MDC kinasusia sherehe hizo katika kile kinachosema ilikuwa wizi mkubwa wa kura uliofanywa na chama cha Zanu-PF, kwa hivyo sherehe hii bila shaka itazongwa na siasa.Mugabe bado hajaapishwa kwa muhula wake wa saba akitawala Zimbabwe, kwa sababu ya kesi ya MDC mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

MDC kilisema kina ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa wizi wa kura ulitokea na kwamba kulikuwa na visa vingine vilivyohujumu matokeo ya uchaguzi huo ikiwemo, rushwa , dhuluma na kuvurugwa kwa daftari la wapiga kura.

WATU 44 WAUWAWA KINYAMA


Takriban waumini 44 wameuawa kwa kupigwa risasi wakiwa msikitini Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, kwa mujibu wa maafisa wa jimbo la Borno. Mauaji hayo yalifanyika wakati wa maombi ya asubuhi Jumapili , ingawa taarifa zimejitokeza Jumatatu , kutokana na hitilafu ya mawasiliano kwani jimbo hilo liko chini ya sheria ya hali ya hatari.

Washambulizi wanasemekana kuwa wanachama wa kundi la wapiganaji la Boko Haram, ambalo liliwaua maelfu ya watu tangu mwaka 2009.Shambulizi lilifanyika katika mji wa Konduga, ulio umbali wa kilomita 35 kutoka mji mkuu wa jimbo hilo , Maiduguri.

Gazeti la Daily Post, liliripoti kuwa watu wengine 26 walikuwa wanatibiwa kwa majeraha waliyopata wakati wa shambulizi hilo hospitalini Maiduguri. Mwanachama wa kikundi cha vijana kinachotoa ulinzi kwa raia, aliambia shirika la habari la Associated Press, kuwa wapiganaji wao wannne waliuawa walipojaribu kutoa kilio cha kutaka usaidizi. Raia wengine kumi na wawili, waliuawa katika kijiji cha Ngom kinachopakana na Maiduguri.

Rais Goodluck Jonathan alitangaza sheria ya hali ya hatari katika majimbo matatu Kaskazini Mashariki mwa nchi mnamo mwezi Mei wakati wanajeshi walipofanya operesheni dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu.Boko Haram linapigania eneo la Kaskazini mwa nchi likitaka kujitawala kwa kutumia sheria za kiisilamu.  Mwandishi wa BBC mjini Lagos, anasema kuwa wakati kundi hilo limekuwa likishambulia makanisa, pia limekuwa likishambulia misikiti.

Habari za mashambulizi hayo zilijitokeza wakati kanda ya video ya kiongozi wa kundi hilo Abubakar Shekau, ilipotolewa akidai kundi hilo kuhusika na mashambulizi hayo ikiwemo kushambulizi dhidi ya vituo vya polisi na kambi za jeshi.

WAFUASI WA MORSI WATAWANYWA MISRI



Polisi nchini Misri, wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji wanaomuunga mkono rais aliyeondolewa mamlakani Mohammed Morsi wakati wa maandamano yao mjini Cairo.Vikosi vya usalama viliingilia maandamano hayo baada ya wafuasi wa Morsi kukabiliana na mahasimu wao wa kisiasa.

Morsi aliondolewa mamlakani na viongozi wa jeshi mwezi Julai kufuatia maandamano makubwa sana.Walioshuhudia vurugu hizo walirushiana mawe na chupa huku watoto na wanawake wakikimbilia usalama wao.Tangu hapo jeshi limeweka serikali ya mpito.

Wafuasi wa Morsi aliyeingia mamlakani baada ya vuguvugu la kiisilamu la Brotherhood kushinda uchaguzi wa rais, wanakataa kukubali serikali mpya ya mpito wakisisitiza kuwa lazima rais wao arejeshwe mamlakani. Vurugu za Jumanne zilianza wakati wafuasi wa Morsi, walipotembea hadi sehemu moja ya Cairo ambako watu wengi wanapinga vuguvugu la Muslim Brotherhood.

Waandamanaji hao walijaribu kuingia katika ofisi za wizara moja ingawa polisi waliwalazimisha kuondoka kwa nguvu.Wakaazi wa eneo hilo walianza kuwakejeli waandamanaji na hapo ndipo polisi walipoingilia mzozo huo.Mamilioni ya wamisri waliandamana kumtaka Morsi aondolewe mamlakani ingawa wadadisi wanasema kuwa kuondolewa kwake kunaonekana kuzorotesha migawanyiko ya kisiasa iliyoko kwa sasa.

Wafuasi wake wamekuwa wakipiga kambi mjini Cairo wakitaka arejeshwe mamlakani. Maafisa wa usalama walitishia kuondoa mahema waliyoweka wafuasi wa Morsi ambako wamekuwa wakipiga kambi lakini wakabatili uamuzi wao baada ya kuamua kuuakhirisha.

Monday, August 12, 2013

NEY ATAFUTWA

MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini Ney wa Mitego, ameweka wazi kuwa ikitokea amefariki dunia hatohitaji kamati kwa ajili ya kuendesha mipango ya msiba wake, kwa kile anachodai kuwa kamati hizo zipo kwa ajili ya kuvuna pesa.

Hayo aliweka wazi baada kupokea ujumbe mfupi kwenye simu yake wenye vitisho uliotokana na mashairi alioimba kwenye single yake mpya ya 'Salaam zao' .

Ujumbe huyo wa vitisho ambao umepokelewa na msanii huyo umekuja mara baada ya msanii huyo kuachia single yake hiyo ambapo mmoja ya mashahiri ni juu ya hela za rambirambi zilizopatikana katika msiba wa msanii Ngwear pamoja na Kanumba kushindwa kuwafikia walengwa.

Akizungumza na jarida la Maisha, mara baada ya kutuma ujumbe alioupokea wa vitisho kwenye ukurasa wake wa 'Instagram', Ney wa Mitego aliweka wazi kuwa amepokea ujumbe wa vitisho mara baada ya kuachia nyimbo hiyo.

Alisema kuwa amepokea ujumbe mbalimbali ambazo zipo zinazowataja wahusika moja kwa moja wale waliohusika kula rambirambi, huku wengine wakimtumia ujumbe wa kumtisha kwa kile alichokiimba katika nyimbo hiyo.

"Mimi hata ikitokea nakufa leo sihitaji mtu yeyote yule anaweka kamati ya mazishi yangu kwani najua kitakachotokea siyo mazishi bali ni kula hela na rambirambi hizo kushindwa kutimiza malengo kama yalivyokusudiwa" alisema Ney wa Mitego.

Aliongezea kuwa hawezi kuacha kuimba ukweli hata kama ataendelea kupokea vitisho, msanii huyo ameachia single yake mpya inayokwenda kwa jina la Salaam zao.

BAKWATA YATAKA UCHUNGUZI WA PONDA


Baraza la waisilamu Tanzania limeunga mkono kauli ya Jumuiya ya taasisi za kisilamu za kuitaka serikali kuchunguza kwa kina tukio lililopelekea kupigwa risasasi kwa mhubiri wa kiisilamu Sheikh Issa Ponda.

Taarifa imetolewa na kaimu mufti wa Tanzania Al Had Musa Salum. Pamoja ya kwamba (BAKWATA) limekuwa likipingana na misimamo ya Sheikh Ponda limesema serikali ilikuwa na nafasi ya kumkamata Ponda kwa kufuata mkondo wa sheria.

Kwa mujibu wa mwandishi wa habari zilizopatikana mjini Dar es Salaam, Baruan Muhuza, sheikh huyo ambaye amekuwa katika mivutano ya mara kwa mara na serikali ya nchi hiyo alipigwa risasi baada ya kutokea vurugu kwenye mkutano wa mawaidha ya baraza la sikukuu ya Idd el Fitr.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Alhajj Mussa Kundecha, amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam  kuwa endapo serikali haitachukua hatua itakayowaridhisha Waislamu, wataamua kufikiria upya mustakabali wao na serikali ya Tanzania.

Sheikh Ponda amelazwa katika hospitali ya taifa, Muhimbili, mjini Dar es Salaam akiuguza jeraha la risasi huku akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu.

Msemaji wa Jeshi la polisi, Advera Senso ameiambia alisema kuwa jeshi lake kwa kushirikiana na jukwaa la haki jinai wameunda kikosi kazi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tukio hilo huku akikana kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi na polisi.

Senso amewalaumu wafuasi wa Sheikh Ponda kwa kuwazuia askari kumkamata Sheikh huyo kwa kuwarushia mawe; hatua iliyosababisha askari hao kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya na hata hivyo wafuasi hao walifanikiwa kumtorosha kiongozi huyo wa kidini.

Taarifa za jumuiya hiyo ambayo inajulikana zaidi Tanzania kama Shura ya Maimamu zinasema kuwa Sheikh Ponda ambaye polisi wanasema walikuwa wakimtafuta kwa tuhuma za kutoa matamko ya uchochezi, alisafirishwa usiku kutoka mji wa Morogoro hadi Dar es Salaam zaidi ya kilomita 200.

Sheikh Ponda kwa sasa anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja alichohukumiwa mapema mwaka huu baada ya kukutwa na makosa kadhaa ikiwemo uchochezi wa kuharibu mali za watu.

RAIS MUGABE AHUTUBIA KWA MARA YA KWANZA


Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe anatarajiwa kutoa hotuba yake ya kwanza tangu kushinda uchaguzi mkuu wa Zimbabwe zaidi ya wiki moja iliyopita.Mugabe atahutubia umma wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya mashujaa mjini Harare kuwakumbuk wale waliofariki wakipigania uhuru wa taifa hilo.
Chama hicho kimewasilisha malalamiko yake kuhusu uchaguzi mkuu ambao kinasema ulikumbwa na wizi wa kura kikitaka uchaguzi huo kurejelewa.Chama pinzani cha MDC, chake waziri mkuu Morgan Tsvangirai, kitasusia sherehe hizo.

Bwana Mugabe alishinda 61% ya kura kwenye uchaguzi huo uliokamilika tarehe 31 mwezi Julai, huku mpinzani wake Morgan Tsvangirai akichukua nafasi ya pili kwa 35% ya kura zilizopigwa.

Chama cha Mugabe Zanu-PF kilishinda wingi wa viti vya bunge kikipata zaidi ya thuluthi mbili ikiwa ni viti 160 ya viti kati ya 210 vya bunge zima.

Sherehe za kuadhimisha siku ya mashujaa Zimbabwe, ni sherehe za kujivunia kwa wazimbabwe wakati ambapo nchi hiyo ilijipatia uhuru wake miaka ya sabini.

Hii leo Mugabe atatoa hotuba yake ya kwanza katika eneo la kumbukumbu la vita hivyo na ambako baadhi ya wapigania uhuru wamezikwa.

Hotuba za Mugabe zinasifika zaidi kwa siasa zake kali za kizalendo, na ambazo zaidi hulenga mkoloni wake wa zamani Uingereza na pia anatarajiwa kujipiga kifua kufuatia ushindi wake mkubwa katika uchaguzi mkuu uliopita mwezi jana.

Chama cha MDC kinasusia sherehe hizo katika kile kinachosema ilikuwa wizi mkubwa wa kura uliofanywa na chama cha Zanu-PF, kwa hivyo sherehe hii bila shaka itazongwa na siasa.
Mugabe bado hajaapishwa kwa muhula wake wa saba akitawala Zimbabwe, kwa sababu ya kesi ya MDC mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
MDC kilisema kina ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa wizi wa kura ulitokea na kwamba kulikuwa na visa vingine vilivyohujumu matokeo ya uchaguzi huo ikiwemo, rushwa , dhuluma na kuvurugwa kwa daftari la wapiga kura.

TNG YATAMBULISHA SINGLE YAO MPYA

 Kundi la TNG la muziki wa bongo fleva nchini wakijiandaa kupanda jukwaani kwa ajili ya kutambulisha nyimbo yao mpya iliyokwenda kwa jina la 'Crazy Love katika ukumbi wa Dar Live jijini Dar es Salaam siku ya Idi Mosi

 Msanii anayeunda kundi la TNG Chiwaman (kulia) akiwa sambamba na kiongozi wa kundi la Wanaume family pamoja na Rose Ndauka ambaye ameshirikishwa kwenye nyimbo ya Crazy Love ambayo ilitambulishwa usiku huo



Monday, August 5, 2013

WAFUASI WA MDC WADAI KUSHAMBULIWA ZIM



Siku moja baada ya Rais Robert Mugabe na Zanu PF kutangazwa kushinda uchaguzi Mkuu nchini humo, baadhi ya wafuasi wa upinzani kutoka chama cha MDC wanasema wameshambuliwa na wenzao wa ZANU PF.

Baadhi ya dola za Magharibi ikiwa ni pamoja na Marekani na Uingereza, zimetilia shaka iwapo uchaguzi huo ulifanyika kwa uwazi. adai hayo yanakuja siku moja baada ya matokeo rasmi ya uchaguzi uliofanyika Jumatano kutolewa na kumpa ushindi rais Robert Mugabe. Chama chake Zanu-PF kilipata thuluthi tatu ya viti vya bunge.

Watu 11 mjini Harare na wengine 20 kutoka mkoa wa Mashonaland, wanasema kuwa walishambuliwa na wafuasi wa Zanu-PF wanaojulikana sana baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.

WATUHUMIWA WATESWA NA POLISI

Washtakiwa wanne wanaokabiliwa na kesi ya wizi wa kutumia silaha wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kutokuwa na imani na afya zao kutokana na mateso waliyoyapata kwa polisi wa kituo cha Oysterbay wakati wa kuchukuliwa maelezo.

Washitakiwa hao ni Ally Hashimu, Donald Nzwenka, Michael Pascal, Kulwa Adamson na Yohanna, watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo wiki iliyopita na baada ya kusomewa makosa yao mawili yanayowakabili mbele ya wakili wa serikali Flora Massawe mbele ya Hakimu Aloyce Katemana

Walidai kwa Hakimu Katemana kuwa hawana imani na afya zao kwani walipigwa na polisi hao wakati wa kuchukuliwa maelezo na kulazimishwa kukubali makosa wasiyoyafanya na mmoja wa washtakiwa hao, alisema kuwa ameingizwa msumari sikioni hivyo hasikii vizuri pamoja na kumkata na panga kwenye ncha za vidole vya miguu.

SELENA GOMEZ AFICHUA SIRI YA BIEBER


Ripoti kwamba Selena Gomez na Justin Bieber wanarudiana na kuachana mara kwa mara zimepata ufumbuzi kutoka kwa kimwana huyo.

"Nimemfahamu Bieber kwa muda mrefu na tunafurahiana kampani ya kila mmoja wetu mara kwa mara " alisema Selena aliliambia Associated Press aliongezea kuwa " mimi niko single na ninafurahia hilo"

MAREKANI YAFUNGA BALOZI ZAKE AFRIKA KASKAZINI


Marekani imesema kuwa itafunga balozi zake kadhaa Kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya kati hadi Jumamosi wiki ijayo kwa sababu ya hofu ya kushambuliwa na makundi ya wapiganaji wa kiisilamu.Balozi 21 za Marekani na ofisi zake zilifungwa Jumapili.

Uingereza ilisema kuwa Ubalozi wake nchini Yemen utasalia kufungwa hadi mwishoni kwa sherehe za siku kuu ya IDD siku ya Alhamisi na kufunguliwa siku ya Jumanne.Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema kuwa kufungwa kwa balozi hizo ni kutokana na serikali kuchukua tahadhari kubwa na wala sio jibu lake kwa tisho jipya la mashambulizi.
Wakati huohuo, balozi za Marekani katika miji ya Algiers, Kabul na Baghdad ni miongoni mwa zile zitakazofungwa na kutarajiwa kufunguliwa Jumatatu wiki ijayo.

AUWAWA BAADA YA KUMNYONGA MKE WAKE

Mwanaume mmoja mkazi wa kijiji cha Kisangwa kata ya Mcharo wilaya ya Bunda mkoa wa Mara, Batule Masanja anadaiwa kumuua mkewa wake kwa kumnyonga shingo kwa kutumia mikono yake kisha na yeye kuuwawa na wananchi wenye hasira kali.

Tukio hilo lilithibitishwa na polisi wilayani hapo, lilitokea usiku wa kuamkia juzi katika kijiji cha Kisangwa kata ya Mcharo kwenye sherehe ya ufunguzi wa nyumba ya ndugu yao.

Friday, August 2, 2013

WASHUKIWA WA UGAIDI KULIPWA FIDIA KENYA



Mahakama nchini Kenya, imeamuru waathiriwa kumi na moja waliohamishwa kinyume na sheria kwa madai ya kuwa washukiwa wa ugaidi walipwe fidia, Walikuwa sehemu ya idadi kubwa zaidi ya washukiwa wa ugaidi waliohamishiswa nchi ya kigeni kinyume na sheria.

Mahakama kwa hivyo imeamuru serikali ya Kenya kuwalipa fidia ya kima cha dola 460,000 waathiriwa wa kitendo hicho.Washukiwa hao walikamatwa mwaka 2007 na kuhamishiwa hadi Somalia na wengine wakipelekwa Ethiopia ili kuhojiwa na mashirika ya kijasusi ikiwemo FBI na CIA.Waathiriwa hao walikuwa miongoni wa washukiwa zaidi ya 100 wa ugaidi waliozuiliwa nchini Ethiopia.

Waathiriwa hao wakiwemo wakenya wanane na raia wawili wa Tanzania pamoja na raia mmoja wa Rwanda, walikamatwa katika ufuo wa bahari nchini Kenya na maafisa wa usalama kabla ya kupelekwa kwa lazima nchini Somalia na hatimaye Ethiopia.

CWT YATOA TAMKO WALIMU KUFELI

RAIS wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, amesema matokeo mabaya ya walimu yaliyotangazwa na Baraza la Mtihani Tanzania (NECTA) hayashangazi kwani walishaiambia serikali iwe innapeleka vyuoni wanafunzi wenye ufaulu mzuri lakini haifanyi hivyo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mukoba alipozungumza na waandishi wa habari alisisitiza kuwa pamoja na kupigia kelele suala hilo, lakini serikali imekuwa ikiendelea kupeleka wanafunzi wabovu hivyo imevuna ilichopanda.

Alisema kuwa matokeo hayo pia yamechangiwa na serikali kutosikiliza madai yao kwani tangu mwaka jana walimu na serikali wamekuwa na ugomvi usiokuwa na majibu.

Aliongeza kuwa madai ambayo walikuwa wakiyadai ni pamoja na nyongeza ya asilimia 100 ya posho ya kufundishia, asilimia 50 ya mazingira magumu, lakini hadi sasa wamepewa nyongeza ya asilimia 8 tu ya nyongeza ya mshahara.

"Ukipanda ujinga unalima uzuzu, sio mara ya kwanza hali hii inatokea,Serikali imeendelea kuziba kwa suala nyeti kama hili la elimu huku ukitarajia taifa kwenda mbali" alisema Mukoba.

WANAFUNZI 30 WAJAZWA MIMBA ROMBO

Wanafunzi 30 kutoka shule mbalimbali za sekondari katika wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro walishindwa kuendelea na masomo katika kipindi cha mwaka 2012 kutokana na kupata ujauzito.

Wanafunzi hao ambao walikatisha masomo wengi wao wanaelezewa kuwa walikuwa kidato cha nne hivyo kujikuta wakitia doa ndoto zao kutokana na kutoendelea na masomo.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari ofisini kwake Ofisa Elimu wa sekondari katika wilaya ya Rombo, Juma Kinanda alisema kati ya wanafunzi hao 30 wanafunzi 28 ni kutoka shule za sekondari za serikali na wawili kutoka shule binafsi.

Kinanda alisema tatizo la mimba shuleni bado ni tatizo ambalo limekuwa likisababisha baadhi ya watoto wa kike kukatisha masomo, na hivyo kuishia kuishi maisha ya mitihani baada ya ndoto zao kuzimika.

Aidha aliweka wazi kuwa tatizo hilo limezidi kuwa kubwa na baadhi ya wazazi kutoshtushwa na hali hiyo na kuona ni jambo la kawaida huku wengine wakidiriki kukataa kutoa ushirikiano pindi watoto wanapobainika kupata ujauzito.