Friday, September 13, 2013

UN WAISHANGAA TANZANIA KUFUKUZA WAKIMBIZI

Umoja wa Mataifa umesema kuwa takriban wakimbizi elfu 25 kutoka Burundi wameondoshwa Tanzania kwa nguvu katika mwezi mmoja uliopita. Afisa wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR amesema malori yanayowasafirisha warundi yamekuwa yakivuka mpaka kila siku , huku wahamiaji haramu wengi wakikosa mahitaji muhimu kama vile maji na chakula

Katika wiki za hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikiwarejesha makwao kwa nguvu wale walioelezwa wahamiaji haramu kutoka Burundi, Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Kwa miaka mingi Tanzania iliwahifadhi mamilioni ya wakimbizi waliokuwa wakiyakimbia mapigano katika nchi jirani . Tanzania kwa upande wake inasema watu hao ni wahamiaji haramu wala sio wakimbizi.

SUALA LA MAPADRI KUOA LAJADILIWA

Suala la mapadri wa Kanisa Katoliki kuoa au la, limeibuka upya na tayari limeanza kuzua mijadala mikali duniani. Mjadala wa sasa umeibuliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican, Askofu Mkuu Pietro Parolin ambaye aliteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo aliposema useja, yaani maisha ya utumishi ndani ya kanisa bila ndoa siyo imani, bali utamaduni na mazoea.

Akizungumzia kauli hiyo, Msemaji wa Vatican, Federico Lombardi alisema kauli ya Askofu Parolin haipingani na mafundisho ya kanisa. Askofu Mkuu Parolin ambaye aliteuliwa karibuni na Papa Francis kushika wadhifa huo kutoka kwa Kardinali Tarcisio Bertone amenukuliwa na Gazeti la El Universal la Venezuela, Amerika ya Kati akieleza kuwa suala hilo linaweza kujadiliwa.

OMBAOMBA, MACHANGUDOA WAKAMATWA

Ombaomba zaidi ya 200 na wasichana wanaofanya biashara ya ngono maarufu kama ‘dada poa’  usiku wa kuamkia jana walikamatwa kwenye operesheni maalumu ya kuwaondoa katika maeneo mbalimbali ya jiji,iliyofanywa kwa ushirikiano wa Polisi na askari wa jiji.

Ombaomba na kinadada hao walikamatwa kwenye Manispaa ya Kinondoni na Ilala ambapo baadaye walihifadhiwa kwenye Viwanja vya Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa(Sabasaba) kabla ya kufikishwa kwenye Mahakama ya Jiji kwa makosa ya uzurulaji.

Wednesday, September 11, 2013

WANAWAKE 26 KILA SIKU KUPOTEZA MAISHA TANZANIA

TWAKIMU za hivi karibuni zinaonesha kuwa Tanzania ni kati ya nchi zinazoongoza kwa idadi kubwa ya vifo votokanavyo na uzazi huku wanawake 26 hupoteza maisha kila siku ambapo vifo hivyo asilimia 19 vinachangiwa na utoaji wa mimba usio salama.

Takwimu hizo ziimetolewa na shirika lisilo la kiserikali Marie Stopes (MST) ambapo iliweka wazi kuwa asilimia 16 tu ya vijana ndio walio katika umri wa uzazi wanatumia njia za kisasa za uzazi wa mpango

ASILIMIA 23 YA WANAUME WAKIRI KUBAKA

Taarifa ya Umoja wa Mataifa kuhusu unyanyasaji dhidi ya wanawake imesema takriban robo ya wanaume wamekiri kubaka japo mara moja.

Hata hivyo kulingana na ripoti hiyo mwanaume mmoja kati ya 10 amekiri kumbaka mwanamke ambaye si rafiki yake. Kwa mujibu wa BBC, Wanaume 10,000 kutoka nchi sita walishiriki katika utafiti huo, nchi hizo ni pamoja na Bangladesh, Sri Lanka, Cambodia, China, Indonesia na Papua New Guinea.

Tuesday, September 10, 2013

ASAP ROCKY AKAMATWA

Mwanamuziki wa hip hop nchini Marekani Asap Rocky amekamatwa na polisi baada ya kumpiga shabiki wake wa kike kwenye tamasha la 'Made in America' lililofanyika huko mjini Philadelphia.

Hayo yametokea baada ya msanii huyo kupita mbele ya mashabiki wake hao waliokuwa wakicheza na kisha mmoja kumshika nguo yake ndipo alipogeuka na kumpiga.

Shabiki huyo ambaye ni mama wa mtoto mmoja, amesema ameumizwa na msanii huyo na teyari ameshamfungulia kesi ya kujeruhi mwimbaji huyo

Sunday, September 8, 2013

AZONTO YAWAPAGAWISHA WABONGO


MSANII wa Ghana mwenye maskani nchini Uingereza Fuse ODG, juzi alifanikiwa kuwateka wakazi wa jiji la Dar es Salaam kwa kufanya shoo ya kihistoria, huku akipandisha mzuka kwa mashabiki waliohudhuria shoo hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ustawi wa Jamii.

Msanii huyo anayetamba na kibao cha Azonto pamoja na Antenna aliweza kuwateka mashabiki wake baada ya kupanda jukwaani hapo na kucheza pamoja na mashabiki miondoko hiyo.

Thursday, September 5, 2013

BUNGE LAGEUKA UWANJA WA VITA

UKUMBI wa Bunge leo uligeuka kuwa ulingo wa ngumi baada ya wabunge wa kambi ya upinzani kutunishiana misuri na askari wa bunge hilo ambapo Kiongozi mkuu wa kambi ya upinzani Freeman Mbowe alipoamliwa kutoka nje na Naibu Spika Job Ndugai.

Hatua hiyo ilitokana baada ya wabunge hao kupiga kura za kukubali au kukataa kuhusu kupitishwa kwa kujadili Mswaada wa Katiba uliopelekwa Bungeni hapo na Serikali ili kuweza kujadiliwa na bunge hilo.

Wabunge hao wa kambi ya upinzani wakiongozwa na Freeman Mbowe walipinga matokeo hayo na kuamua kusimama na wakati huo huo Spika Ndugai aliwataka kukaa chini ili kuendelea na kuchangia hoja za msingi za kujadili mswaada huo.

Wednesday, September 4, 2013

BINTI AMEZA SIMU

WIVU wa kimapenzi umemuweka matatani msichana anayeishi nchini Brazil, Adriana Andrade baada ya kuamua kumeza simu yake ya mkononi ili kumzuia mpenzi wake asisome 'message' katika simu yake.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 19 amejikuta akilazimika kuumeza simu hiyo baada ya kugundua alikuwa na message za ajabu ambazo zingezua utata pindi mpenzi wake angezisoma.

Habari zilizoripotiwa na mtandao wa Hispania Yipeta zilieleza kuwa msichana huyo aliamua kumeza simu yake ya mkononi baada ya mpenzi wake kutaka kusoma message zilizomo katika simu hiyo.

Mtandao huo uliendelea kuripoti kuwa baada ya tukio hilo msichana huyo alilazimika kufanyiwa upasuaji ili kutolewa simu hiyo tumboni mwake.

MAHAKAMA YARUKA KUWAACHIA WASHTAKIWA DAWA ZA KULEVYA


Mahakama Kuu imewatetea majaji na mahakimu dhidi ya tuhuma zilizotolewa kwao kuwa waliwaachia kwa dhamana washtakiwa wa dawa za kulevya kinyume cha sheria na kuwafanya watoroke. Jaji Kiongozi, Fakih Jundu amesema mahakama haipaswi kubebeshwa lawama katika hilo, bali ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kutokana na kutokutimiza masharti ya kisheria wanapofungua kesi mahakamani.

Kauli ya Jaji kiongozi imekuja baada ya shutuma zilizotolewa dhidi yao baada ya chombo kimoja cha habari (jina tunalo) kuandika habari kwa kuwataja kwa majina baadhi ya majaji na mahakama kuwa wamekuwa wakiwalinda washtakiwa wa dawa za kulevya katika kesi ambazo wamekuwa wakizisikiliza.

Shutuma hizo zilihusiana na tukio la hivi karibuni ambapo raia wawili wa Pakistani waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya dawa za kupewa kuachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu na zimekuwepo taarifa kuwa wametoroka nchini.

WACHIMBA MIGODI WAANZA MGOMO AFRIKA KUSINI


Takriban wachimba migodi 80,000 wa dhahabu nchini Afrika Kusini wanatarajiwa kuanza mgomo kudai nyongeza ya mishahara.Chama cha kitaifa cha wafanyakazi wa migodini kinataka waongezwe mishahara kwa asilimia sitini.

Sekta ya madini ya dhahabu ndio moja ya sekta kubwa duniani lakini imekuwa ikikumbwa na misukosuko katika miaka ya hivi karibuni huku ile ya madini ya platinum ikijikwamua kutokana na athari za migomo iliyokumba sekta hiyo mwaka jana.Wafanyakazi hao wiki jana walikataa pendekezo walilopewa la nyongeza ya asilimia 6 ambacho ni kiwango cha mfumuko wa bei kwa sasa.

Inakisiwa kuwa migomo hiyo ya wachimbaji migodi ikiwa itafanyika, itapotezea nchi hiyo zaidi ya dola milioni 30 kila siku.Wamiliki wa migodi wanaonya kuwa migomo hiyo huenda ikasababisha migodi ya dhahabu kufungwa na maelfu kupoteza kazi zao kufuatia kushuka kwa bei ya dhahabu.

Wanasema kuwa gharama za uchimbaji dhahabu zimepanda kwani wamelazimika kutumia pesa nyingi zaidi katika shughuli nzima za uzalishaji, Kwa miezi mingi Afrika Kusini ilikuwa nchi yenye kuzalisha zaidi dhahabu ikiwa inazalisha asilimia 68 ya dhahabu yote duniani katika miaka ya sabini.

PUTIN AMEONYA MAREKANI

Rais wa Urusi Vladimir Putin, ameonya Marekani na nchi za Magharibi dhidi ya kushambulia Syria.Alisema kuwa hatua zozote za kijeshi dhidi ya Syria itakuwa ni uvamizi. Lakini kwenye mahojiano na shirika la habari la Associated Press, kabla ya mkutano wa wiki hii wa G-Twenty mjini St Petersburg, bwana Putin alisema kuwa huenda akaunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa ikiwa kuna thibitisho kuwa silaha za kemikali zilitumiwa dhidi ya raia.Rais wa Marekani Barack Obama ametoa wito wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria baada ya kusema kuwa kuna thibitisho kuwa rais Assad ametumia silaha za kemikali dhidi ya wananchi wake.

Putin pia alipuuza wasiwasi kuwa wanariadha au mashabiki wataadhibiwa ikiwa watatoa matamshi yatakayoonekana kuwa propaganda kuhusu mapenzi ya jinsia moja wakati wa michezo ya olimpiki itakayofanyika nchini humo.

Wakati huohuo , maseneta nchini Marekani wameridhia mswada wa azimio linalompa idhini Rais Barack Obama kutekeleza shambulio la kijeshi dhidi ya Syria. Mswada huo utapigiwa kura wiki ijayo.

MWANAMKE AMEZA HELA

Mwanamke wa kimarekani amelazwa hospitali baada ya kuumia kooni na tumboni wakati akijaribu kutoa kiasi kikubwa cha fedha alizozimeza kwa kutumia ufagio wa kusafisha choo.

Monday, September 2, 2013

MSHINDI REDD'S PHOTOGENTICS APATIKANA

 Mshindi wa Miss Redd's Photogentics (katikati) akiwa amepozi na washiriki waliofanikiwa kuingia tano bora ya miss Photogenitics. Kinyanganyiro hicho kilifanyika juzi katika hoteli ya Giraff Dar es Salaam

RICHI AWA KIVUTO UZINDUZI FOOLISH AGE


MSANII wa filamu nchini Single Mtambalike 'Richi Richi' amekuwa kivuto katika uzinduzi wa filamu ya Foolish Age uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam, baada ya kupanda jukwaani na 'kummwagia' kitita cha fedha msanii mwenzake Elizabety Michael 'Lulu'.

Richi alijikuta akivutiwa na msanii Lulu mara baada ya kuimba kibao cha Yahaya kilichoimbwa na muimbaji Lady Jaydee, mara baada ya kumaliza kuizindua movi yake hiyo ambapo alitoa fursa kwa mashabiki wake waliohudhuria uzinduzi huo kuiangalia kwa dakika 10.

Richi alishindwa kuvumilia mara baada ya kusikia msanii huyo anaimba nyimbo ambayo kwa upande wake inamvutia, hali iliyopelekea kupanda jukwaani na kumwagia kitita cha fedha huku akionyesha kuifurahia nyimbo hiyo.