Thursday, November 28, 2013

ZITTO KABWE APONZWA NA WALAKA


Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema kimesema kwamba kilifikia uamuzi wa kumvua nyadhifa zake, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe kutokana na sababu moja tu ya kuhusika katika Waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013.

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwamba waraka huo unaeleza mbinu za uasi ambazo zililenga kufanya mabadiliko makubwa ya kiuongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho jambo ambalo ni kinyume na katiba, sheria na itifaki za Chadema.

Hivi karibuni, Kamati Kuu ya Chadema iliwavua nyadhifa zao, Zitto, Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kutokana na madai hayo.

Siku tatu zilizopita, Zitto na Dk Kitila waliitisha mkutano wa wanahabari na kueleza sababu mbalimbali za kung’olewa kwao ikiwamo suala la posho na ruzuku za vyama vya siasa.

“Wamefukuzwa katika uongozi kutokana na kuandaa mpango wa mapinduzi uliopo katika waraka wa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013,” alisema Lissu na kuongeza:

“Hawa wote hawakuvuliwa madaraka kwa sababu ya taarifa za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu ukaguzi wa hesabu za chama, suala la posho kwa wabunge wala kuuza majimbo ya uchaguzi mwaka 2010.”


Alisema kutokana na kosa hilo, Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chadema ilikutana juzi kupitia uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu na kuridhika nao, “Leo (jana) wahusika wote watapatiwa barua zao zilizoorodhesha makosa yao kumi na moja wanayotakiwa kujibu ndani ya siku 14.” Bila ya kuyataja, Lissu alisema makosa hayo yote yamejikita katika waraka huo.


Mnyika pia alijibu hoja zilizotolewa na Wakili wa kujitegemea na Diwani wa Kata ya Mabogini mkoani Kilimanjaro (Chadema), Albert Msando juu ya kasoro wakati wa kutoa hukumu kwa makosa ya Zitto na Dk Kitila, ikiwa ni pamoja na kukiukwa kwa katiba ya chama inayoeleza kuwa mtu hatachukuliwa hatua za kinidhamu kabla ya kupewa mashtaka kwa maandishi na mamlaka husika na kupewa nafasi ya kuyajibu kwa maandishi.

Mnyika alisema, “Zitto na Dk Kitila hawakumwambia wakili wao ukweli kwamba kanuni hii ya chama ilishafanyiwa marekebisho muda mrefu na Baraza Kuu la chama na kuongezwa kifungu (d), ambacho kinasema: “Kamati Kuu inaweza kuchukua hatua za dharura kama inaona masilahi ya chama yanaathiriwa.”


Waraka
Mnyika alisema waraka uliowang’oa Zitto na Dk Kitila ambao umechapishwa katika magazeti mbalimbali pamoja na mitandao ya kijamii, siyo ule uliowasilishwa katika Kikao cha Kamati Kuu.

“Waraka utakaotumika katika mashtaka yao siyo huo. Sisi tutautumia ule ambao uliwasilishwa katika Kamati Kuu ambao una mambo makubwa na mengi zaidi kuliko huo unaochapishwa sehemu mbalimbali, ikibidi tutautoa huo waraka halisi,” alisema.

No comments:

Post a Comment