Saturday, July 13, 2013

ZAIDI YA WATANZANIA 250 WAKAMATWA NA DAWA ZA KULEVYA NJE YA NCHI


KAMISHINA wa tume ya kuratibu na kuthibiti madawa ya kulevya Christopher Shekiondo amebainisha kwamba watanzania wengi wanaokamatwa na dawa za kulevya nchi za nje adhabu zao mara nyingi zinakuwa kunyongwa au kifungo cha maisha jela.

Akizungumza kwa simu jana Kamishina huyo alisema, kwa kipindi cha muda wa mwaka mmoja anakumbuka zaidi ya watanzania zaidi ya 250 wamekamatwa katika nchi mbalimbali na dawa za kulevya.


Aliweka wazi kuwa  watu hao zaidi ya 100 wamekamatwa nchini Brazil wakiwa wanadawa za kulevya aina ya cocain kwa ajili ya kusafirisha nchi nyingine.

Kutokana na uzoefu aliokuwa nao ameweka wazi kuwa mara nyingi watu wanaokamatwa na dawa hizo wanaishia kunyongwa, au kufungwa maisha.

Kamishina huyo alifafanua kuwa kuna baadhi ya watu wengine walikamatwa nchini China wakiwa na dawa aina ya Heroine wakijiandaa kusafirisha dawa hizo kwenda nchi mbalimbaili ikiwemo Afrika kusini.

"Mara zote hizo watanzania hao wamekuwa wakikamatwa nje ya nchi wakiwa wanajiandaa kusafirisha dawa hizo, nchi za mbali kwenye matumizi hayo" alisema Shekiondo.

Aliendelea kuweka wazi watu hao wanatumia nchi ya Tanzania kama njia ya kusafirisha dawa hizo ingawa zinabaki chache kwa ajili ya matumizi ya watumiaji wa dawa hizo.

Kutokana na vuguvugu la watu wanaokamatwa nje ya nchi kwa lengo la kusafirisha dawa hazo amebainisha kuwa jumla ya watu zaidi ya 250 wamekamatwa na wengine wameshahukumiwa kulingana na kosa hilo na kutegemea sheria ya nchi.


Hivi karibuni kumekuwa na matukio ya baadhi ya wasanii kutumia madawa ya kulevya na wengine kukiri kuacha kutumia dawa hizo, Shekiondo aliweka wazi kuwa kitengo hicho kilishafanya mahojiano na baadhi ya wasanii hao ambapo walitoa ushirikiano kwa kueleza kuwa wanauziwa dawa hizo na watu wa chini.

Gazeti hili jana liliripoti juu ya wasichana wawili kukamatwa  Afrika Kusini kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya zenye thamani zaidi ya sh. bilioni 6.8 wakitokea Tanzania

Wasichana hao miongoni mwao ni msanii anayeshiriki katika video za wasanii wa muziki wa bongo fleva, Agnes Jerald 'Masogange' pamoja na Melisa Edward

Kamanda wa Polisi Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Geofrey Nzoa, alithibitisha kukamatwa kwa wasichana hao nchini huko ambapo aliwataja wanawake hao kuwa ni Agnes Jerald pamoja na Melisa Edward.

Wakati huo huo kamanda Nzoa alieleza kuwa changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na mbinu wanazotumia katika ubebaji wa dawa hizo kubadilika kila wakati.

"Kila siku wanakuja na mbinu mpya mara wanabeba sehemu za siri, kumeza hivyo kila wakati wanakuja na mbinu mpya ambazo ni changamoto kubwa kwetu ingawa tunajaribu kupambana nazo" alisema Nzoa.





No comments:

Post a Comment