Tuesday, July 30, 2013
PINDA KORTINI ALHAMISI
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimetangaza kumburuta Mahakamani siku ya Alhamisi asubuhi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa kile kinachodaiwa amekaidi kufuta kauli yake ya kuruhusu vyombo vya usalama kupiga wananchi wanaokaidi amri za vyombo hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Maboresho na Utetezi na mwanasheria wa LHRC , Harold Sungusia, alisema wanamfungulia shtaka Waziri Mkuu Pinda, kesi ya kimkakati inayomlazimu ajibu mbele ya mahakama msimamo wa serikali unaomsababisha atoe kauli hiyo.
Katika kikao cha bunge kilichopita wakati wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu alisema, "ukifanya fujo na umeambiwa usifanye hiki na wewe ukaamua kukaidi utapigwa tu, maana hakuna namna nyingine ... eeh maana wote tukubaliane nchi inaongozwa kwa misingi ya kisheria, sasa kama wewe umekaidi hutaki, unaona wewe ni imara zaidi, wewe ndio jeuri zaidi wataka kupigwa tuu mimi nasema muwapige kwa sababu hakuna namna nyingine maana tumechoka sasa "
Sungusia alisema kauli hiyo ya Waziri Pinda ni uvunjaji wa katiba ya nchi na haki za binadamu, hivyo hawataikalia kimya. Alisema walishamtaka afute kauli yake lakini hakufanya hivyo.
Aliweka wazi kuwa pamoja na bosi wake (Rais Jakaya Kikwete) kueleza umma kuwa Waziri wake aliteleza lakini bado LHRC inaona anayo ya kujibu mbele ya Mahakama .
Mwanasheria huyo alifafanua kuwa kauli ya Waziri Pinda ni ukiukaji wa ibara ya 13 ya sheria inayozungumzia usawa mbele ya sheria na ibara ya 30 ibara ndogo ya (3) inayoeleza kama haki ya mtu inavunjwa, imeshavunjwa au inaelekea kuvunjwa unaweza peleka shauli lako Mahakama kuu
"Kwa hiyo LHRC hatutavumilia na kuona haki za raia zinavunjwa kauli ya Pinda ametudhihirishia msimamo wa serikali, hivyo hata waliokuwa wanafanya matukio na kunyanyasa raia (polisi) kumbe walikuwa mgongoni mwake na walikuwa wakilindwa na yeye" alisema Singusia.
Labels:
news
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment