Tuesday, August 27, 2013
CCM YAMTIMUA UWAKILISHI MANSOUR
Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (Nec), jana iliridhia kumvua uanachama, Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi, Mansour Yussuf Himid kutokana na kukiuka miiko ya chama hicho. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuwa Mansour ambaye hivi karibuni alikuwa waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), amefukuzwa uanachama kutokana na kukiuka mambo matatu.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni kushindwa kutimiza malengo ya CCM na kutekeleza malengo ya uanachama, kushindwa kutekeleza wajibu wa uanachama na kukiuka maadili ya uongozi, kuikana na kuisaliti Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015. Kutokana na uamuzi huo, Nape alisema Mansour hatakuwa na nafasi ya kukata rufani mahali popote kwa kuwa uamuzi uliofikiwa jana ni wa kikao cha juu cha mwisho.
Akizungumza jana, Mansour alisema kwa sasa hawezi kuzungumza mengi kwani anahitaji muda wa kutafakari kutokana na uzito wa suala lenyewe. “Ndugu yangu nashukuru sana kwa kunipigia simu. Ila ninahitaji muda wa kutulia kwanza. Nipe kama siku mbili au tatu hivi halafu nitaongea,” alisema Mansour, ambaye amekuwa Mwakilishi wa Kiembe Samaki tangu mwaka 2005.
Nec ilifikia uamuzi huo ikibariki mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Kuu ya CCM upande wa Zanzibar iliyomvua uanachama kutokana na misimamo yake ya kisiasa na hasa suala la Muungano.Mansour aliwahi kushika nyadhifa kadhaa ndani ya CCM ikiwamo ya ujumbe wa Halmashauri Kuu na Mweka Hazina wa chama hicho upande wa Zanzibar.
Kwa mara ya kwanza, tuhuma za Mansour zilifikishwa katika kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM Zanzibar, kilichoketi Agosti 16, mwaka huu katika Ofisi za CCM Kisiwandui ambacho wajumbe wa kamati hiyo kwa kauli moja walitoka na azimio la kumfuta uanachama.
Suala hilo lilifikishwa Kamati Kuu ya CCM, Zanzibar Agosti 22, mwaka huu kupitia uamuzi huo na iliafiki. Kitendo cha Mansour kuingia kwenye Kamati ya Maridhiano ya Zanzibar inayoongozwa na mwanasiasa mkongwe Hassan Nassor Moyo ambayo imekuwa ikipigania Muungano wa mkataba ilichochea tofauti yake na makada wenzake wa CCM Zanzibar.
Kitendo cha kuungana na Mzee Moyo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad kupigia debe suala la Muungano wa Mkataba kati ya Tanganyika na Zanzibar kuliwakera makada wa CCM waliomchukulia kuwa anapingana na Katiba na Ilani ya CCM vilivyosimamia katika Serikali mbili.
Labels:
news
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment