Monday, September 23, 2013

HALI TETE KUOKOA MATEKA JENGO LA WESTGATE KENYA

HUKU  hali ya mshikemshike ikiendelea kushuhudiwa katika jengo la Westgate lenye maduka, ufyatulianaji risasi umesikika ndani ya jengo hilo lenye maduka na migahawa zaidi ya themanini.

Wapiganaji wa Al shabaab wamewateka nyara raia ambao idadi yao haijulikani bado, waliokuwemo ndani ya jengo wakiendelea na shughuli zao kuanzia Jumamosi mchana wakati wapiganaji wa Al shabaab walipowavamia na kuanza kufyatua risasi kiholela.

Inaarifiwa kuwa  kuna miili ya watu kumi waliopoteza maisha katika ghorofa ya kwanza ya jengo hilo, aidha wapiganaji hao wanaoaminika kuwa wanachama wa Al Shabaab ni kati ya kumi na kumi na watano na bado wapo ndani ya jengo hilo.

Ripoti zinasema kuwa ufyatulianaji mkubwa wa risasi pamoja na milipuko imesikika katika jengo hilo kwa takriban dakika 15.

Harakati za kuendelea kumaliza operesheni hiyo zinaendelea lakini hali ya mateka walio ndani ya jengo hilo inaendelea kudorora. Wapo baadhi ya wakenya  waliofanikiwa kuondoka katika jengo la Westgate kwa usaidizi wa polisi.


Rais Kenyatta amesema kuwa jeshi linajitahidi kuhakikisha kuwa linakabiliana vilivyo na wanamgambo hao.

Helikopta za polisi zinazunguka juu ya jengo hilo pamoja na ndege za kijeshi kushika doria. Vikosi vya usalama vinaendelea na operesheni kujaribu kuwanusuru waathiriwa wakati hali ikiwa ikiendelea kuwa tete katika eneo la shambulizi.

Awali jeshi la Kenya lilisema limeweza kudhibiti jengo hilo lote ingawa bado limetaja hali kuwa tete mno hasa katika kujaribu kuwaokoa mateka waliosalia ndani ya jengo hilo.

Ripoti zinasema kuwa watu 69 wamefariki katika shambulizi hilo la Al Shabaab kufikia sasa huku 175 wakijeruhiwa.

Baadhi wametibiwa na kuondoka hospitalini. Baadhi ya majeraha waliyopata ni majereha ya risasi na kutokana na guruneti ambalo Al shabaab waliwarushia wale waliokuwa ndani ya migahawa siku ya Jumamosi.

Kundi hilo limekiri kutekeleza shambulio hilo kutokana na hatua ya Kenya kupeleka majeshi yake nchini Somalia ili kukabiliana na wapiganaji hao.

No comments:

Post a Comment