Wednesday, September 18, 2013

SERIKALI YASHINDWA NA UHALIFU WA TINDIKALI


Matukio ya kumwagiwa tindikali yameendelea kukithiri huku Serikali ikiendelea kutoa ahadi za kudhibiti bila mafanikio. Hivi karibuni baada ya raia wawili wa Uingereza kumwagiwa tindikali Zanzibar, Serikali iliweka mikakati mikali ya kudhibiti matumizi ya kemikali hiyo, lakini bado matukio hayo yameendelea kuwepo.

Tukio la kumwagiwa tindikali kwa Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Cheju, Mkoa wa Kusini Unguja, Joseph Mwang’amba ni mwendelezo wa uhalifu huo ambao Serikali imeshindwa kabisa kuudhibiti. Akieleza jinsi tukio hilo lilivyotokea, Padri Mwang’amba anasema alikuwa nje ya duka linalotoa huduma za mawasiliano ya mtandao (Sun Shine Internet Caffee) liliopo eneo la Mlandege Wilaya ya Mjini Unguja, ndipo alipotokea kijana mmoja na kumwagia tindikali.

Wakati Padri huyo akieleza hayo, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, ameijia juu polisi kwa kushindwa kudhibiti matukio ya viongozi wa dini na Serikali visiwani humo, kushambuliwa kwa kumwagiwa tindikali huku akilitaka kuwakamata waliohusika na tukio hilo.

Kiongozi huyo wa dini, aliyejeruhiwa maeneo ya usoni, mikononi na kifuani baada ya kumwagiwa tindikali hiyo alisafirishwa jana na ndege ya kukodi ya Shirika la Coastal kutoka visiwani humo hadi Dar es Salaam na baadaye kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi. Kwa upande wake, Padri wa Parokia ya Mtakatifu Joseph, Zanzibar, Thomas Assenga aliyefuatana na kiongozi huyo mpaka MNH, alisema siku za nyuma Padri Mwang’amba alitolewa vitisho na mtu ambaye hamfahamu wakati akienda kutoa huduma katika kituo cha wazee cha Welezo.

Alisema kabla ya kufika kituoni hapo, kuna eneo ambalo nyakati za asubuhi watu hufanya mazoezi barabarani ambapo kuna mtu mmoja alimtolea maneno ya vitisho. Tukio hilo linafuatia tukio la Agosti 7, mwaka huu ambapo raia wawili wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kirstie Trup (18) walimwagiwa tindikali katika maeneo ya Mji Mkongwe, Zanzibar na vijana wawili waliokuwa wakiendesha pikipiki aina ya Vespa. Waingereza hao walisafirishwa siku tatu baadaye kurudi kwao Uingereza kwa ajili ya matibabu.

Wakati huo huo Siku tano baada ya tukio la Waingereza hao kumwagiwa tindikali, Serikali kupitia vyombo vyake vya uchunguzi iliwataka wananchi kuisaidia kuwafichua na kutoa ushahidi wa uhalifu huo kwani ni vigumu kuwabaini wahusika.

Kauli hiyo ilitolewa kwa pamoja jana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) Eliezer Feleshi, katika mkutano wao na waandishi wa habari, uliolenga kueleza mikakati ya kupambana na matumizi yasiyo sahihi ya tindikali nchini.

No comments:

Post a Comment