Friday, September 13, 2013

SUALA LA MAPADRI KUOA LAJADILIWA

Suala la mapadri wa Kanisa Katoliki kuoa au la, limeibuka upya na tayari limeanza kuzua mijadala mikali duniani. Mjadala wa sasa umeibuliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican, Askofu Mkuu Pietro Parolin ambaye aliteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo aliposema useja, yaani maisha ya utumishi ndani ya kanisa bila ndoa siyo imani, bali utamaduni na mazoea.

Akizungumzia kauli hiyo, Msemaji wa Vatican, Federico Lombardi alisema kauli ya Askofu Parolin haipingani na mafundisho ya kanisa. Askofu Mkuu Parolin ambaye aliteuliwa karibuni na Papa Francis kushika wadhifa huo kutoka kwa Kardinali Tarcisio Bertone amenukuliwa na Gazeti la El Universal la Venezuela, Amerika ya Kati akieleza kuwa suala hilo linaweza kujadiliwa.


Hata hivyo, msimamo huo unaweza kupingwa na waumini wengi wenye misimamo mikali ndani ya kanisa hilo ambao bado wanaamini kuwa kuishi useja ndiyo mfumo na utamaduni unaofaa ndani ya kanisa hilo.

Kwa upande wake, Papa Francis mwaka jana hata kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, alizungumzia suala hilo kwa maneno mafupi kuwa angependa kuona mfumo huo ukibaki kama ulivyo.

Msimamo huo wa Askofu Mkuu Parolin unamaanisha kuwa kuna haja ya kanisa hilo kufanya mabadiliko makubwa kwenye kanuni ngumu ya useja kwa mapadri wake.

“Useja si suala la kitaasisi, lakini linaonekana kuwa kweli, linaaminika. Ni suala gumu ambalo linaweza kujadiliwa kwani si imani ya kanisa (dogma), halihusu imani ya kanisa,” alisema Askofu Mkuu Parolin.

Askofu huyo alisema kwa kuwa siyo suala la kiimani, useja katika kanisa hilo limezama zaidi kwenye utamaduni.


No comments:

Post a Comment