Sunday, September 22, 2013

VYAMA VYA UPINZANI VYATIKISA DAR


Vyama vya upinzani jana vilifanya mkutano mkubwa kuwashawishi wananchi kupinga kile walichokiita kuhujumiwa kwa mchakato wa Katiba Mpya, wakitangaza Oktoba 10 kuwa siku ya Watanzania wote kushiriki katika maandamano kushinikiza wapewe haki ya kuandaa Katiba yao.

Wakizungumza kwa kupokezana katika Viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam jana, wenyeviti wa vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF, walieleza kuwa wataendelea kushirikisha taasisi za kiraia kupinga hujuma dhidi ya mchakato wa Katiba Mpya na kwamba hawatakubali endapo Rais Jakaya Kikwete atasaini Muswada wa Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba Mpya.

Akizungmza katika mkutano huo Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba alisema chama chake hakitakubali endapo Rais Kikwete atasaini muswada huo kwa kuwa una lengo la kupata Katiba Mpya isiyokuwa na tija kwa taifa. Alisema kuwa Katiba inayoandaliwa ni kwa ajili ya Watanzania wote na siyo kundi la watu, hasa CCM na kwamba mchakato wa kuwapata wajumbe 166 wa Bunge la Katiba kutoka makundi mbalimbali siyo sahihi.

“Haiwezekani kila taasisi ikateuwa wajumbe tisa ambao majina yao yatakwenda kuchakachuliwa na usalama wa taifa, kisha kupata majina ya watu wanaowataka wao, kitu hiki kama CUF hatutakubali,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:

“Hatutarudi nyuma na kukubali kuendelea na mchakato huu endapo Rais atasaini muswada huu. Tutaendeleza harakati za kupinga kwani bila hivyo tutapata Katiba Mpya isiyokuwa na tija.”


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kuwa ni wakati wa kukaa meza moja ya mazungumzo kuondoa tofauti zilizopo ili kulinusuru taifa kuingia katika machafuko.

Alisema kama taifa, linatakiwa kujifunza kutoka mataifa mengine yalivyotokea maafa katika michakato ya kuandikwa kwa Katiba Mpya.

“Ni wakati wa kukaa meza moja, kwa kushirikisha wadau mbalimbali kwani Katiba inayotafutwa ni ya Watanzania wote na siyo ya CCM,” alisema Mbatia na kuongeza:

“Lazima tupate Katiba Mpya kwa gharama yoyote ile, iwe ndani au nje ya Bunge ili kuhakikisha tunapata Katiba ya Watanzania wote.”

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alisema kosa kubwa katika kudai haki ni woga na hatutapata Katiba Mpya kama tutaendelea kuwa taifa la watu wenye hofu. Tunataka kukutana na makundi mbalimbali katika jamii ambayo ni viongozi wa dini, wasomi na watu wa makundi mengine kuwaeleza kinachoendelea sasa hivi.

Hata migogoro ya kiimani baina ya Wakristo iliyotokea nchini imesababishwa na katiba iliyopo sasa, kama Rais atasaini wao hawatashiriki Bunge la Katiba na watatumia kila mbinu iliyopo duniani kuueleza umma nini kimetokea na hawataendelea kunyenyekea vitisho vya Jeshi la Polisi.

Tunalaani mchakato wa katiba kuhodhiwa na chama kimoja na tunatangaza Oktoba 10, mwaka huu kuwa ni siku maalumu ya kudai katiba na sasa hawataenda tena Ikulu kwani inaaminika huko ni kwenda kunywa chai na watatangaza maandamano nchi nzima.

No comments:

Post a Comment