Katika wiki za hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikiwarejesha makwao kwa nguvu wale walioelezwa wahamiaji haramu kutoka Burundi, Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Kwa miaka mingi Tanzania iliwahifadhi mamilioni ya wakimbizi waliokuwa wakiyakimbia mapigano katika nchi jirani . Tanzania kwa upande wake inasema watu hao ni wahamiaji haramu wala sio wakimbizi.
Takriban watu milioni moja walitoroka kutoka Burundi na kuingia Tanzania wakati wa mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe wakati vita vilipozuka mwaka 1993. Wengi walirejea kwa hiari wakati amani ilipopatikana mwaka 2006. Nchi hiyo imekuwa makao kwa mamilioni ya wakimbizi katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi iliyopita kutokana na migogoro katika eneo la maziwa makuu.
Maafisa wa Tanzania sasa wameanza kutekeleza amri ya kuwaondoa kwa nguvu wale wanaodaiwa kuwa wahamiaji haramu kutoka Burundi, Rwanda, na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo. Shughuli hii imetokea wakati mmoja na mgogoro wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Rwanda ambayo imekuwa ikikanusha madai ya kuchochea vurugu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mgogoro ndani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo nao unaendelea kuchochea idadi ya wakimbizi wanaotoroka vita na kuingia katika nchi jirani.
No comments:
Post a Comment