Thursday, September 19, 2013

KESI YA DAWA ZA KULEVYA YAWATOA JASHO MAWAKILI



Kesi ya dawa za kulevya inayomkabili raia wa Kenya, Mwanaidi Ramadhani Mfundo, maarufu kwa jina la Mama Leila au Naima Mohammed Nyakiniwa na wenzake wanane, imeendelea kugubikwa na utata wa kisheria na kuzua mvutano uliosababisha iahirishwe kwa mara nyingine ili kusubiri uamuzi wa Mahakama Jana, Mahakama Kuu ilitengua hoja iliyozua mvutano mkubwa juzi kwa kuruhusu upande wa mashtaka kuwasilisha notisi ya kuongeza shahidi muhimu kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Eva Mamuya jambo lililopingwa na upande wa utetezi.

Mbali ya Mama Leila, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Anthony Arthur Karanja na Ben Ngare Macharia (wote Wakenya). Wengine ni Watanzania watano, Sarah Munuo, Almas Said, Yahya Ibrahim, Aisha Kungwi, Rajabu Juma Mzome na John William. Wakati upande wa utetezi ukipinga uamuzi huo wa jana, upande wa mashtaka ulitoa hoja nyingine ya kuongeza shahidi wa pili, ASP Neema na kuibua mvutano mkali wa kisheria uliomlazimu Jaji Grace Mwakipesile anayesikiliza kesi hiyo, kuiahirisha hadi Ijumaa wiki hii atakapotoa uamuzi kama upande wa mashtaka ulikuwa sahihi au la kuwasilisha notisi hiyo mahakamani kabla ya uamuzi wa jana.

Ubishi ulianza mapema mahakamani wakati Jaji Mwakipesile alipokuwa akijiandaa kusoma uamuzi wake juu ya maombi ya upande wa mashtaka kuwasilisha notisi ya kuongeza shahidi. Wakili wa utetezi, Yassin Member alisimama na kumwomba jaji kutokusoma uamuzi wake kwani tayari walikuwa na notisi ya upande wa mashtaka ya kuongeza ushahidi wakati ni kinyume cha sheria.


Member alilalamika kuwa upande wa mashtaka uliomba kuongeza shahidi mmoja lakini notisi ilionyesha walikuwa wanataka kuongeza mashahidi wawili. “Mheshimiwa tunaomba usisome kwani tunashangaa tayari tumepewa notisi ya upande wa mashtaka wakati ukiwa bado hata hujatoa uamuzi wa maombi yao ya kuwasilisha notisi ya kuongeza shahidi. Kibaya zaidi wanataka kuongeza mashahidi wawili na siyo mmoja,” alisema Member.

Jaji Mwakipesile alijibu kwa kutaka upande wa utetezi kuipa nafasi mahakama kutoa uamuzi wake wa maombi ya upande wa mashtaka yaliyosababisha kesi hiyo kuahirishwa juzi. “Ipe nafasi Mahakama kutoa uamuzi wake wa ombi la upande wa mashtaka la kuahirisha kesi ili waweze ku-file notice (kuwasilisha taarifa) ya additional witness (shahidi wa nyongeza), jambo ambalo ninyi mlipinga,’’ alisema Jaji Mwakipesile na kisha kutoa uamuzi wake na kukubali upande wa mashtaka kuongeza shahidi.


Uamuzi huo ulisababisha mvutano mkali mawakili wa utetezi wakisema haikuwa sahihi kwa upande wa mashtaka kuongeza mashahidi wakati ulishindwa kwenye Mahakama za chini wakati wa usikilizwaji wa mwanzo.

No comments:

Post a Comment